Google PlusRSS FeedEmail

BUSHOKE: WASANII WENGI WANAOENDA AFRIKA KUSINI WANABEBA MADAWA YA KULEVYA



Kama ulidhani Watanzania waishio nchini Afrika Kusini wana kazi na maisha mazuri, basi ulikosea kwani kama huna elimu ya kutosha ukaamua kuzamia nchini humo ni lazima utaishia katika mikono isiyo salama.


Ruta Bushoke, ambaye alitamba na kibao cha “Mume Bwege”, anasema maisha wanayoishi Watanzania wengi, hususan wasanii, ni ya kusikitisha.


Akizungumza na Starehe visiwani Zanzibar wakati wa tamasha la filamu la ZIFF, Bushoke alisema wengi wao wanaishi kwa kutegemea biashara ndogondogo, ambazo hazina faida kubwa huku wengi wao wakiishia kubebeshwa mizigo ya dawa za kulevya na wafanyabiashara wakubwa kutoka nchi mbalimbali, hasa Tanzania.


“Watanzania wengi wanajihusisha na biashara za mihadarati, ile siyo nchi ya kwenda kichwa kichwa kwa sababu watu wengine wana vyeti vizuri, lakini wamekosa kazi. Labda itokee bahati na kule unakutana na mataifa ambayo huwezi kukutana nayo sehemu yoyote,” anasema Bushoke.


Msanii huyo anasema wengi wanapenda kuzamia bila kujua akifika kule atafanya shughuli gani, wengine wanatamani maisha mazuri kwa kuyatazama juu juu lakini ni magumu.


“Kazi wanazoweza kufanya wazamiaji ni kuuza vitu vidogovidogo kama simu, samani au kitu chochote kilichoibwa, pia uuzaji wa dawa za kulevya kama bangi,” anasema Bushoke.


Kwa mujibu wa Bushoke, wengi wanajishughulisha na uuzaji wa dawa za kulevya kwa kutuma watu na wengine wakisafirisha.


Akizungumzia maisha yake nchini Afrika Kusini, Bushoke ambaye ni mtoto wa mtangazaji Max Bushoke ambaye alikuwa nyota wa muziki wa dansi nchini, anasema mipango yake ilikuwa kuishi kwa mwaka mmoja.


“Kule mimi ni nyumbani, nilikuwa sijaenda kwa ajili ya kufanya kazi ila nilikwenda kifamilia kwa kuwa wazazi wanaishi kule. Nilipanga kwenda kukaa mwaka mmoja lakini nikajikuta nakaa miaka mitatu.”


“Sikupoteza chochote kwa sababu baba yangu yupo kule na alizidi kunifundisha mambo ya muziki kwa kuwa amenitangulia na anajua zaidi yangu. Kwa hiyo muda mwingi tulikuwa tunaongea habari hizo na kunielewesha kuhusu muziki wa kimataifa,” anasema Bushoke.


Hata hivyo, Bushoke anasema akiwa nchini humo aliona fursa mbalimbali zinazohusu sanaa, lakini kila alipojaribu hakufanikiwa ingawa kikubwa alichojifunza ni kuhusu soko la kule na namna nafasi zinavyopatikana ili azitumie muda mwafaka.


Anasema akiwa Afrika Kusini amefanya kazi mbalimbali za muziki ambazo ataziachia baada ya kupata usimamizi mwingine hapa nchini.


“ Baba yangu akienda kazini nilikuwa nabaki nyumbani kwa sababu mama yangu anaishi Pretoria na baba Johannesburg. Kila siku nilibaki studio ndogo pale nyumbani najifunza kupiga vyombo vya muziki mbalimbali,” anasema.


Akizungumzia machafuko yaliyotokea Afrika Kusini yaliyohusisha wenyeji kushambulia wageni kwa madai kuwa wanawachukulia ajira zao, Bushoke anasema ingawa kipindi hicho hakuwa nchini humo, amejifunza kuwa wazawa wamekuwa na dhana potofu kuhusu wageni.


“Ni kitu ambacho sikishangai sana kwa Afrika Kusini kwa sababu tunaishi nao tunawajua jinsi wanavyofikiria wao na matatizo ambayo wameyapitia,” anasema.


“Tunapozungumza nao wanatuambia wao walitawaliwa na wazungu, baada ya kupata uhuru walitegemea kwamba mambo yangekuwa mazuri, lakini kumbe pamoja na uchumi mkubwa wa nchi yao, vitu vingi bado wanavimiliki weupe.”


Anasema kuwa kwa mtu wa kawaida, bado maisha yao ni ya chini kiuchumi na yanaonekana yanazidi kuwa magumu kadri siku zinavyokwenda ndiyo maana kunaibuka chuki dhidi ya wageni.

This entry was posted in

Leave a Reply

    Powered By Blogger

    Receive all updates via Facebook. Just Click the Like Button Below...

    Get This SpiceUpBlogging