Utata kuhusiana na mshiriki wa shindano la muziki la Tusker Project Fame kutoka nchini Rwanda, Jackson Kalimba ambaye anadaiwa kuwa ni mwanamuziki anayetambulika, hivyo hafai kushiriki shindano hilo linalohusisha wanamuziki chipukizi hatimaye umeingia katika hatua nyingine ambapo video ya wimbo wake sasa imewekwa mtandaoni.Hata hivyo, waandaaji wa shindano hilo kampuni ya Endemol tawi la Nairobi wametoa taarifa kwa washiriki wa shindano hilo pamoja na wadau wa muziki wa Afrika mashariki na kati ya kwamba wao bado wanaridhishwa na Jackson kuwa na uhalali wa kushiriki shindano hilo.
Katika taarifa iliyosainiwa kwa niaba ya timu nzima ya Endemol na kusainiwa na Winnie Onyach ambaye ni Afisa uhusiano wa kampuni ya Ogilvy ambao ni wasimamizi wa kitengo cha habari cha shindano hilo, wamebainisha kwamba juu ya kwamba jackson alipata bahati ya kurekodi video, bado kijana huyo ambaye anaelekea kukonga nyoyo za mashabiki hajawahi kuwa na kipato kupitia muziki kwa hiyo haisababishi yeye kuitwa mwanamuziki rasmi."Mwanamuziki ambaye hahitajiki kushiriki Tusker Project Fame ni ambaye anajulikana na ameshawahi kufanya maonesho na kujiingizia kipato kupitia muziki jambo ambalo Jackson hajawahi katika maisha yake ya muziki," ilisema taarifa hiyo.Kufuatia vigezo hivyo, Jackson anabaki bado kuwa mshiriki halali wa Tusker Project Fame na atakuwa akisailiwa na Majaji kama wenzake na iwapo wataridhika na ushiriki wake pia ni halali kwa mwanamuziki huyu kuwa mshindi.