JAYMOE ASHANGAZWA BAADHI YA WASANII WANAOTUMIA MADAWA KUTAFUTA UMAARUFU
MSANII wa muziki wa kizazi kipya nchini miondoko ya Hip Hop, Jumaa Mohamedy 'Jaymoe Mchopanga' amewashangaa baadhi ya wasanii kutafuta umaarufu kwa kutumia madawa ya kulevya.
Akizungumza na jarida hili Jaymoe aliweka wazi kuwa anashangazwa na baadhi ya wasanii hao kutumia madawa ya kulevya hali ambayo inapelekea kushusha hadhi ya tasnia yao ya muziki wa kizazi kipya.
Alisema kuwa hapo awali tasnia hiyo iikuwa haina sifa ya wasanii kutumia madawa ya kulevya ila sasa kutokana na baadhi ya wasanii kutafuta umaarufu hivyo wanajikuta wanatumia madawa ya kulevya.
"Ni bora kuwa na mademu wengi kuliko kutumia madawa ya kulevya kwani utumiaji wa madawa hayo yanaaribu dira na mfumo wa maisha kiujumla" alisema Jaymoe.
"Hapo mwanzo fani hii ilikuwa inasifika kuwa na wasanii mabishoo lakini tofauti na kipindi hiki ambacho kumeibuka na hili tatizo la baadhi yao kutumia madawa ya kulevya huku wakiamini kuwa ili uwe bora kimuziki lazima utumie madawa hayo jambo ambalo halina tija kwenye fani yetu" alisema Jaymoe.
Pamoja na hayo Jaymoe aliongezea kuwa anampango wa kubadili mfumo mzima wa mazingira ya wasanii ili kuokoa kizazi ambacho kimejikita kwenye matumizi ya madawa ya kulevya kwani kwa kufanya hivyo anaamini ataokoa kizazi pamoja na muziki wa kizazi kipya.








