Msanii huyo aliimba nyimbo hiyo na Jaydee wakati wa uzinduzi wa filamu yake ya kwanza tangu atoke jela kwa dhamana aliyoipa jina la Foolish Age ambapo uzinduzi huo ulifanyika katika ukumbi wa Mlimani City Dar es Salaam .
Msanii huyo alianza kuimba kiitikio cha wimbo huo akiwa Back Stage, ambapo aliwashangaza watu pale alipomudu vyema wimbo huo, hali iliyosababisha msanii Single Mtambalike 'Richi Richi' kushindwa kuzuia hisia zake na kuamua kupanda jukwaani hapo kumtunza kitita cha fedha msanii huyo.
"Jamani kumbe muziki unalipa ile mbaya nimeimba ubeti mmoja tu hapa ona hela kibao, kuanzia sasa na mimi nitaanza kuimba muziki" alisema Lulu.
Akiizungumzia filamu hiyo Lulu aliweka wazi kuwa foolish age ndicho kipindi cha ukuaji ambacho kila mmoja anapitia na ndipo vijana wengi wanaharibikiwa kimaisha.
Hivyo anaamini kuwa filamu hiyo imezungumzia ukweli ambao unamgusa kila mmoja, hata kama haujamtokea yeye lakini imeshawahi kumtokea ndugu au katika jamii yake inayomzunguka.
Msanii huyo alijinadi kuwa yeye ndiye msanii bora wa kike kwa mwaka 2013-2014 baada ya kupokea tuzo hiyo iliyotolewa na Ziff mwaka huu.
"Mimi ndiye msanii bora wa kike kwa mwaka huu jamani hii siyo tuzo za vichochoroni ni tuzo inayotambulika kila mahali nchini ni kutoka Ziff naamini kipaji changu na bado nitaendelea kufanya vizuri" alijinadi Lulu.
Uzinduzi huo ulisindikizwa na Bendi ya Machozi ambapo mwanamuziki Judith Wambura 'Lady Jaydee' alikuwa kivuto kwa kuweza kuzikonga nyoyo za mashabiki waliojitokeza mahali hapo hali iliyopelekea kuleta ushindani kwa mashabiki wake kumtunza hela jukwaani hapo.








