Mrembo muigizaji ambaye ni raia wa Kenya, Lupita Nyong’o Jumamosi (February 22) aling’aa katika tuzo za NAACP Image na kushinda tuzo ya muigizaji bora msaidizi wa kike ‘Outstanding Supporting Actress’ kwa ushiriki wake kwenye filamu ya 12 Years a Slave.
Lupita aliweza kuwashinda wasanii wakubwa waliokuwa wanachuana nae katika kipengele hicho akiwemo Alfre Woodard, mshiriki wa Long Walk to Freedom Naomie Harris, Octavian Spencer na malikia wa talk show Oprah Winfrey.
Baada ya kutangazwa kuwa mshindi katika kipengele hicho katika utoaji wa tuzo hizo zilizofanyika Pasadena, California, Lupita aliitaja tukio hilo kwake kuwa tukio la kihistoria.
“Umekuwa mwaka wa kihistoria katika filamu kwa sisi sote katika chumba hiki, na najivunia kuwa sehemu ya historia hiyo.” Alisema Lupita Nyong’o. “Ni heshima kutambuliwa kwa filamu yenye maana kubwa kwa watu wengi.”
Huo ulikuwa usiku wa furaha kwa wahusika wengi wa filamu ya 12 Years A Slave, kwa kuwa mbali na Lupita Nyong’o, muongozaji wa filamu hiyo Steve McQueen alishinda tuzo ya muongozaji bora, mwandishi wa filamu hiyo pia John Ridley aliibuka mwandishi bora wa filamu.








