TYRESE AZINDUA FILAMU INAYOELEZEA MAISHA YAKE
Mwanamuziki maarufu Tyrese Gibson mwishoni mwa wiki iliyopita, Machi 31 amezindua filamu ijulikanayo kama “ A Black Rose That Grew From The Concrete” yaani “Ua waridi jeusi lililostawi katika zege”, inayoelezea maisha yake na vipindi vigumu alivyopitia utotoni katika kitongoji cha Watts, jijini California, kabla ya kuwa mwanamitindo, mwanamuziki na hatimaye mcheza filamu maarufu.
Nyota ya Tyrese ilianza kuonekana mwaka 1995 baada ya kushinda shindano la kusaka vipaji lililoandaliwa na kampuni ya Coca Cola na hivyo kupata nafasi kuigiza tangazo la kinywaji cha Coca Cola na baadae kushiriki katika Filamu ya “Baby Boy” mwaka 2001 akishirikiana na gwiji wa filamu Ving Rhames na mwanamuziki Snoop Doggy.
Tyrese mwenye umri wa miaka 34, mpaka sasa ametajwa mara 2 kugombea tuzo za Grammy na ametoa vibao vingi vilivyotamba kwenye chati za muziki za billboard kama vile : “Sweet Lady”, “How you gonna act like that”, “Stay”, na “Lately”, na hivi karibuni ameshiriki katika filamu zilizofanya vizuri kimauzo kama Transformers na Fast & Furious.
Tyrese pia amecheza filamu za Flight of the phoenix (2001), Four Brothers (2005), Annapolis , Waist deep ( 2006), The Take , To each this Own na Death Race (2008)
Mbali na muziki na filamu Tyrese ameandika vitabu viwili ambavyo ni , ‘How To Get Out of Your Own Way’ na ‘Manology’ alichokitoa mwaka huu kwa kushirikiana na Mchungaji Run ambaye alikuwa ni miongoni mwa ma rapa wakongwe waliounda kundi la Run DMC lililotamba sana miaka ya 80 na 90.
Hivi sasa Tyrese amejikita zaidi kwenye filamu na albamu yake ya mwisho aliitoa mwaka 2011 iliyojulikana kama “Open Invitation” iliyobeba kibao cha “Stay,” kilichoshika namba 1 kwenye chati za muziki za billboard na kumfanya atajwe kuwa miongoni mwa wagombea tuzo ya grammy kundi la albam bora ya R&B.