HATIMAYE ule utata wa muda mrefu ulioibuka baada ya kijana Brandon Howard kudai kuwa Michael Jackson ndiye baba yake mzazi, vipimo vya DNA vimeonesha kuwa huo ni ukweli kwa asilimia 99.9.
Brandon ambaye alikuwa akitambulika kuwa ni mtoto wa Miki Howard, mwimbaji wa nyimbo za injili aliyekuwa rafiki wa Michael Jackson na alikuwa akizunguka nae mara kadhaa kwenye ziara na matamasha yake na alikuwa anawakilishwa na baba yake Michael Jackson, Joe Jackson miaka ya 1980.
Taarifa za vipimo vya DNA ziliwekwa wazi na daktari wa meno na upasuaji wa Beverly Hills, Dr. Joseph Goodman alipofanya mkutano na vyombo vya habari Alhamisi wiki hii ambapo alifungua bahasha na kusoma matokeo ya DNA yanayoonesha kuwa Michael ni baba mzazi wa Brando kwa asilimia 99.9.
“I think we have the proof.” Alisema daktari huyo.
Hata hivyo, chanzo kimoja kiliiambia Daily News ya Marekani na kusisitiza kuwa Brandon sio mtoto wa Michael Jackson bali ni mtoto wa baba yake Michael, mzee Joe Jackson.
Wakati vuguvugu linaendelea, mwimbaji anaejulikana kwa jina la Augie Johson amejitokeza na kudai kuwa Brandon ni mtoto wake yeye na kwamba ana vielelezo vyote na yuko tayari kuviweka wazi na hata kuchukuliwa vipimo vya DNA.
Michael Jackson alifariki na kuacha watoto watatu wanaofahamika ambao ni Prince Michael (16), Paris (15), na Blanket (11).
Inasemekana kuwa Brandon ndiye mtoto ambaye Michael Jackson alimuimba kwenye wimbo wake wa ‘Billie Jean’.
Baada ya kushambuliwa na baadhi ya watu kuwa alikuwa anataka tu kupata matunzo kama mtoto wa Michael Jackson huku mwanasheria wa Michael akisisitiza kuwa hawajawahi kusikia hata Michael akimtaja, Brandon aliandika kwa urefu maelezo yanayoonesha kuwa hakuwa na sababu ya kutafuta huduma kama mtoto wa Michael Jackson kwa kuwa hata hapo alipo anatunzwa vizuri.