Wikiendi hii kutakuwa na tukio moja tu kubwa la burudani Dar es Salaam, Tanzania. Kiwanja ni Dar Live, Mbagala Zakhem, Dar ambako msanii mkali, Jean Pierre Nimbona ‘Kidum’, atapiga mzigo wa nguvu Kidum, ili kuwaonesha Watanzania yeye ni nani kwenye muziki.
“Nimewaambia waandaaji wa hilo onesho kuwa nataka muda mrefu. Nitafanya kazi kubwa sana, nakuja na vifaa vyangu kwa ajili ya kuhakikisha nawapa Watanzania hasa wakazi wa Dar es Salaam burudani ya uhakika.“Nakuja Dar es Salaam nikiwa na timu yangu kamili. Nimedhamiria kukata kiu ya mashabiki wangu, kwa hiyo siku hiyo ni kazi moja. Mashabiki wangu wa Dar es Salaam wasikose,” alisema Kidum.
Katika onesho, staa wa Bongo Fleva, Sunday Mangu ‘Linex’, atakuwepo kuwasha moto, naye amepania kumuonesha Kidum kwamba yeye ndiye mchawi wa sauti ya Kiafrika.Muziki wa Taarab, watampata malkia wao, kwani Khadija Kopa amejipanga kufanya shoo ya nguvu akiwa na kundi la Tot Taarab.Kwa upande wa dansi, itakuwepo bendi ya Mliman Park Orchestra ‘Sikinde’ ambayo itateremsha ngoma za kale na mpya.








