WHITNEY HOUSTON DIED AT THE AGE 48.
MWANAMUZIKI na mcheza filamu nyota kutoka Marekani Whitney Houston amefariki dunia jijini Los Angeles akiwa na umri wa miaka 48. Katika taarifa ya polisi kuhusiana na kifo cha mwanamuziki huyo imesema Houston amefariki akiwa chumbani kwake katika Hoteli ya Baverly Hilton ambapo alipanga kama mgeni hotelini humo. Houston alikuwa ni mmoja wa wanamuziki wa kike waliojipatia umaarufu mkubwa katika kipindi chote akiwa na vibao vilivyojipatia umaarufu mkubwa ikiwemo kibao cha I Will Always Love You na Saving My Love For You. Lakini katika kipindi cha karibuni maisha yake ya kimuziki yalikumbwa na misukosuko mikubwa kutokana na ndoa yake na mwanamuziki Bobby Brown pamoja na utumiaji wa dawa za kulevya. Msemaji wa polisi Mark Rosen aliwaambia waandishi wa habari kuwa Houston alifariki majira ya saa tano za usiku kwa majira ya Afrika mashariki ambapo maofisa kutoka kitengo cha zimamoto pamoja na walinzi wa hoteli hiyo walikuwa wakijaribu kuokoa maisha yake. Chanzo kamili cha kilichopelekea kifo cha mwanamuziki huyo bado hakijawekwa wazi lakini Rosen amesema kuwa hakuna dalili yoyote kwamba mwanamuziki huyo ameuwawa.