Wasanii wawili wa muziki wa Hip Hop Bongo, Ibrahim Musa ‘Roma’ na Emanuel Simwinga ‘Izzo Business’, nusura warushiane makonde kwenye mkutano wa waandishi wa habari, uliofanyika Bamaga, Mwenge, Dar es Salaam, Wasanii hao ambao mara kwa mara wamekuwa wakirushiana maneno ya kuudhi na kejeli kwenye vyombo vya habari, walikuwa kwenye mkutano wa utambulisho kwa waandishi wa habari kuhusu pambano lao la jukwaani, Jumapili hii kwenye Ukumbi wa Dar Live, Mbagala Zakhem, Dar.
Kivumbi kilianza kutimka wakati wasanii hao walipopewa nafasi ya kueleza chanzo cha ugomvi wao ambapo bila kujali eneo walilokuwepo, kila mmoja alianza kuporomosha maneno ya kuudhi na majigambo kwa mwenzake.
Izzo Bussines ndiye aliyekuwa wa kwanza kuhamaki, hivyo kutaka kumvaa Roma ambaye wakati huo alikuwa anaporomosha majigambo yake kwa mwenzake, akimfananisha na mzoefu wa kutumia gesti za uswahilini, kwa hiyo hawezi kulingana na yeye anayelala hoteli za kitalii.
Awali, kabla ya sintofahamu hiyo kutokea, Meneja wa Matukio Dar Live, Abdallah Mrisho alisema kuwa Jumapili hii, Izzo na Roma, watapambana jukwaani kumtafuta mkali wa Hip Hop kati yao, hivyo kuachana na tambo za mitaani.“Wakipambana jukwaani itasaidia kuwapa burudani mashabiki wao na pale ndiyo atajulikana mkali hasa ni nani, badala ya kuendelea na malumbano yasiyokwisha,” alisema Mrisho na kuongeza:“Mbali na pambano la Izzo na Roma, siku hiyo kutakuwa na onesho la nguvu kati ya Jahazi Modern Taarab na Mashauzi Classic, wakati muziki wa dansi kutakuwa na Bendi ya Akudo Impact, vilevile Kassim Mganga ‘Tajiri wa Mahaba’ atakuwepo.