TAASISI ya mawasiliano (TCRA) imeiomba Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) kuhamasisha wasanii kuongeza na kuboresha vipindi vyao ili viweze kuleta maendeleo ya nchi katika tasnia ya sanaa na utamaduni.
Ombi hilo limetolwea na Mhandisi mwandamizi wa masafa TCRA Bw. Joel Chacha katika kongamano lililohusu teknolojia ya dijitali na faida zake katika sekta ya sanaa na wasanii lililowasilishwa kwenye jukwaa la sanaa liliofanyika jijini Dar es Salaam jana.Bw. Joel alisema katika mabadiliko ya utangazaji kutoka analojia kwenda dijitali sekta ya sanaa na wasanii nchini watafaidika kwa kutangaza kazi zao za usanii na kuutangaza utamaduni wa mtanzania ndani na nje ya nchi."Kupitia mabadiliko haya sanaa, Tanzania itapata soko kwa njia iliyo rahisi na kuwatangaza wasanii nje ya mipaka yetu pamoja na kuutangaza utamaduni wetu na pia wasanii watapata ajira mbalimbali kutokana na kuongezeka kwa makampuni ya sanaa.", alisema.Mbali na faida hizo baadhi ya wasanii waliohudhuria kongamano hilo wameulalamikia mfumo huo mpyA kutokana na changamoto watakazo kumbana nazo ikiwemo upoteaji wa kazi zao za filamu na utamaduni wa Mtanzania."Kupitia mfumo wa dijitali ambao unalenga kutumia ving'amuzi itakuwa rahisi kwa mtu wa nje ya nchi kuiba sanaa zetu kwa kunyonya kazi zetu na kwenda kutumia katika nchi zao,"alifafanua Bw.Surchyang Raphael ambaye ni msanii na Mwenyekiti wa TASA Ilala.Naye msanii kutoka katika kikundi cha Kashkash Bw. Amos Beda aliulalamikia mfumo huo kwa kusema kwamba mfumo huo ni wa gharama sana kwa mwananchi wa kawaida kuweza kuumudu katika kununua king'amuzi na kulipia gharama za uendeshaji.Wakiongezea katika changamoto za mfumo wa dijitali waliiomba TCRA kusimamia kudhibiti mfumuko wa bei ya ving'amuzi na pia kudhibiti uingiaji wa aina tofauti za ving'amuzi ili iwe rahisi kwa mwananchi kumiliki king'amuzi kiurahisi zaidi ambacho kitaonyesha chaneli zote.Aidha waliiomba serikali izidi kutoa elimu kwa wanachi kuhusu mfumo mpya wa dijitali na matumizi ya ving'amuzi kwani inaonekana wananchi walio wengi hawana elimu ya kutosha juu ya mfumo huu.Mfumo wa dijitali ulizinduliwa rasmi Agosti 2011 na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ambao ulienda sambamba na uzinduzi wa nembo ya dijitali kwa ambao utekelezaji wake unatarajiwa kuanza rasmi Januari 2013.