MREMBO WA EAST AFRICA KUPATIKANA OKT. 14
Mrembo atakayeiwakilisha nchi katika mashindano ya mwaka huu 'Miss East Africa' atatangazwa rasmi Oktoba 14, mwaka huu katika hoteli ya Serena, Dar es salaam.
Jumla ya warembo 148 wameomba kuiwakilisha nchi katika mashindano ya hayo, lakini ni Mrembo mmoja tu atakayechaguliwa kuiwakilisha nchi katika mashindano hayo makubwa ya urembo katika ukanda huu wa Africa na yanayosubiriwa kwa hamu na wapenzi wa fani hiyo ndani na Nje ya Africa Mashariki.
Mashindano hayo yanatarajiwa kufanyika Desemba 7, mwaka huu katika ukumbi wa Mlimani City,Dar es salaam.
Wakati huohuo nchi ya Burundi imebadili mwakilishi wake ambapo sasa itawakilishwa na mrembo Ariella Kaneza (23), Mwanafunzi wa mwaka wa pili wa chuo Kikuu cha Universte De Lumiere.
Taarifa kutoka Burundi iliyosainiwa na Mratibu wa Mashindano ya Miss East Africa nchini humo, Serge Nkurunziza, zimeeleza kwamba Burundi imeamua kubadili mwakilishi wake ili kuhakikisha kwamba nchi hiyo inashinda taji hilo kwa mara ya pili tangu mashindano hayo yalipoanzishwa mwaka 1996 ,baada ya kugundua kwamba mwakilishi wake wa awali anapungukiwa baadhi ya sifa chache za kuweza kunyakua taji hilo.
Burundi imewahi kushinda taji hilo mara moja mwaka 2008 kupitia kwa mrembo wake Miss Claudia Niyonzima, mashindano ya Miss East Africa mwaka huu yanatarajiwa kuwa na mvuto wa aina yake na yatashirikisha warembo kutoka nchi 16 za ukanda wa Afrika Mashariki.
Nchi zilizothibitisha kushiriki mashindano hayo ni wenyeji Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi, na nchi nyingine zilizoalikwa kushiriki ni Ethiopia, Eritrea, Somalia, Djibouti, Southern Sudan, Malawi na visiwa vya Seychelles, Madagascar, Reunion, Comoros, na Mauritius.
Mashindano ya Miss East Africa yanalenga kukuza ushirikiano na kutangaza utamaduni wa Afrika Mashariki, pamoja na kutangaza utalii wa Tanzania kama nchi wenyeji wa mashindano hayo makubwa katika ukanda huu wa Afrika.
Mashindano ya Miss East Africa yanamilikiwa na kuandaliwa na kampuni ya Rena Events Ltd ya jijini Dar es salaam.