TAMASHA LA MUZIKI WA DANSI LEO FM ACADEMIA, MSONDO, AKUDO HAPATOSHI
Tamasha kubwa la muziki wa dansi nchini ambalo litashirikisha bendi mbalimbali maarufu, linatarajiwa kufanyika leo na kesho katika viwanja vya Leaders, Dar es Salaam.
Bendi hizo ni DDC Mliman Park 'Sikinde', Msondo Ngoma, B-Band ya Banana Zoro, Mashujaa, Akudo Impact, FM Academia na Wazee Sugu chini ya King Kikii 'Sugu'.
Akizungumza Dar es Salaam jana Mratibu wa tamasha hilo, Edwin Ndege alisema maandalizi ya tamasha hilo yamekwenda vizuri, na lengo la tamasha hilo ni kukisaidia Chama cha Muziki wa Dansi Tanzania (CHAMUDATA) kwa ajili ya kuboresha chama chao.
"Ni tamasha la aina yake ambalo halijawahi kutokea nchini na huu ni mwanzo tu, kwani tumepanga kila mwaka tuwe tunalifanya, na tutaongeza bendi nyingine zaidi na pia tumelenga kuwasaidia CHAMUDATA," alisema Ndege
Katika tamasha hilo kiingilio kitakuwa ni sh. 20,000 kwa viti maalum na sh. 5,000 kwa viti vya kawaida, ambapo bendi ya Isha Mashauzi Classic pamoja na Khadija Kopa watasindikiza tamasha hilo.
Alisema kwa kutambua umuhimu wa tamasha hilo wanaimani kubwa kuwa, mashabiki watafurika kwa wingi, ili kujionea bendi hizo zitakapokuwa zikitumbuiza huku kila moja ikionesha umahiri wake.
Baadhi ya viongozi wa bendi hizo zitakazoshiriki tamasha hilo litakaloanza leo, wamewasifu waandaaji, huku wakisisitiza kuwa liwe linafanyika mara kwa mara.
Kwa upande wake kiongozi wa bendi wa Wazee Sugu King Kikii, alisema kuwa amefurahishwa na waandaaji wa tamasha hilo, ambao wamebuni kitu ambacho kitaufanya muziki wa dansi usisahaulike, kama ilivyo sasa huku wasanii wa bongo flava wakitamba kwa sasa.
"Muziki wa zamani una radha yake sio kama ilivyo sasa watu wanachukulia muziki kama kitu rahisi sana, lakini muziki wa zamani hadi leo kuna bendi ambazo zinauendeleza na kila mahali zinapigwa," alisema King Kikii.
Tamasha hilo limedhaminiwa na Radio Times FM, Global Publishers, Business Times, Real Star, Whindhok, Fly 40, Face to Face Bar na Push Mobile.