PRODYUZA chipukizi kwenye tasnia ya muziki wa kizazi kipya nchini Emanuel Maungu anajulikana pia kwa jina la E.M.A theboy ameweza kukaa siku nne bila ya kulala kutokana na kuwa na mapenzi na kazi yake hiyo
Hali hiyo ilimtokea baada ya kubanwa na kazi nyingi za kurekodi nyimbo za wasanii akiwemo Recho huku akiwa hataki kulimbikiza kazi nyingine na kuikosea kazi yake
Akizungumza na mwandishi wa habari hii E.M.A theboy alisema kuwa aliweza kukaa siku nne bila ya kulala kutokana na kubanwa na kazi nyingi za kurekodi huku akiwa anajifunza baadhi ya vitu vipya kwa ajili ya kuboresha kazi yake
"Siwezi kuisahau siku hizo kwa kutoweza kupata usingizi siku nne mfululizo nikiwa niko muda wote studio narekodi huku pia nikigawa muda wa kujifunza vitu vipya ambavyo kila siku vinakuja ili niweze kuwa tofauti na wengine na kutengeneza muziki wenye ubora" alisema E.M.A theboy
Nyota huyo anayekuja kwa kasi kwenye tasnia hii alisema kuwa baada ya miaka miwili muziki wa bongo fleva utabadilika kwani mashabiki watataka kusikia nani anaimba nini na muziki umetengenezwa kwa kiwango, hivyo ni wakati wa wasanii kubadilika kwa kujifunza ili wawe bora zaidi
E.M.A theboy ni prodyuza anayekuja kasi kwenye tasnia hii kutoka THT ambaye teyari ameshatengeneza nyimbo mbalimbali zinazofanya vizuri kwenye tasnia hii ya muziki wa kizazi kipya huku akiibua ushindani kutoka kwa maproducer wengine








