WASANII WAFUNGUKA SWALA LA KUTUMIA 'NDUMBA'
Msanii wa muziki wa kizazi kipya nchini Nasibu Abdul 'Diamond Platnum' baada ya kukumbwa na kashfa nzito za kutumia ushirikina ili nyota yake iweze kung'araa na kuwa na mashabiki wengi kwenye tasnia hiyo baadhi ya wasanii wazungumza juu ya tuhuma hizo
Dully Sykes ni mmoja wa wasanii wa bongo fleva ambaye amezungumza juu ya tuhuma hizo kwa upande wake alisema hawezi kuwaamini waganga wa kienyeji kwani walio wengi ni waongo
Kutokana na uongo wao na kutoaminika katika jamii wametumia njia ya kumtumia msanii Diamond kama kivuli cha wao kupata fedha kwa sababu teyari amefanikiwa katika maisha kupitia sanaa ya muziki
Dully aliendelea kufunguka juu ya jambo hilo na kusema kuwa baadhi ya watu wanaroho za ajabu na hali hiyo inawapelekea kufanya tendo lolote baya kwa mtu bila ya kufikiria linamadhara gani
"Mimi ni msanii ambaye ninafanya vizuri tangu naanza muziki mpaka sasa na mbona siambiwi kama natumia uchawi, siamini uchawi na bado nipo juu na ninafanya vizuri kwenye 'gemu' wamuache mtoto wa watu kama mungu amumfungulia kwa muda huu wamuache anajitafutia rizi yake" alisema Dully
Pamoja na hayo Dully alieleza kuwa wapo baadhi ya wasanii ambao wanafanikiwa kwa kutumia ushirikina na mpaka inafikia hatua ya kufanya hilo ni kwa sababu hawana vipaji na kujiamini
Aliongezea kuwa kunasababu gani ya kuendelea kumshtumu msanii huyo wakati anafanya vizuri na kuweza kuendeleza maisha yake, kutokana na hilo Dully aliwataka watanzania kuendelea kutoa ushirikiano wao ili muziki uendelee kufika mbali
Kwa upande wake Barnaba ambaye pia ni msanii wa kizazi kipya alisema kuwa yeye humwamini mungu kwa kila jambo hivyo kwake hakuna nafasi ya ushirikina na hajui unafaida gani
Alisema msanii Diamond kuonekana anafanya vizuri ni wakati wake umefika kwani swala la muziki pia linaendana na muda na wakati wa mtu kuwa juu kutokana na kazi nzuri anazofanya
Aliongezea kuwa haamini kuwa kung'aa kwa msanii huyo kumetokana na kutumia ushirikina bali ni wakati wake umefika na watanzania wamekubali kazi yake ndio maana anafanya vizuri
Pamoja na hayo Barnaba alisema kuwa anaamini kile anachokifanya na anakiheshimu anachokifanya kwani muziki kwake ni kazi hivyo juhudi ndizo zinazomfikisha hapo alipo
Diamond ni msanii wa muziki wa kizazi kipya anayetamba na nyimbo Nataka kulewa amekumbwa na kashfa ya kumtumia mganga wa kienyeji ili aweze kufanya vizuri katika muziki wa bongo fleva ambapo mganga huyo amezungumza katika baadhi ya vyombo vya habari








