Tamasha la muziki la kimataifa ambalo hufanyika kila mwaka la
‘World Music Day’ linafanyika leo (Ijumaa) katika viwanja vya posta Kijitonyama
jijini Dar es Salaam ambapo wanamuziki Kala Jeremiah, Ben Paul, bendi ya Twanga
pepeta na wengineo wanaotamba katika tasnia ya muziki nchini watalipamba
tamasha hilo.
Tamasha hilo ambalo limeandaliwa na Umoja wa Ulaya wa taasisi
za utamaduni (EUNIC) zikiwamo Aliance France-Dar es Salaam, Goethe
Institut-Tanzania na British Council linalenga kutoa fursa kwa wanamuziki
wakongwe na wachanga kukutana katika jukwaa hilo la kimataifa kutoa burudani
hiyo kwa wapenzi na mashabiki wa muziki.
Mratibu wa Tamasha hilo ambalo limedhaminiwa na Fasjet, Abel
Shuma ambaye pia ni Mratibu wa Shughuli za Utamaduni Alliance France Dar es salaam
amewataja wasanii watakaotumbuiza katika tamasha hilo kuwa ni pamoja na Msanii
wa Reggae nchini Jhiko Man, Barnaba na bendi yake, Ben Paul na Twanga Pepeta
Wengine ni Msanii bora wa mwaka na msihindi wa tuzo tatu za
KTMA Kala Jeremiah, Godzila, Super Maya Baikoko, Makini Kids na wengine wengi
ambao watajumuika kwa pamoja kunogesha tamasha hilo ambalo hufanyika Juni 21
kila mwaka katika nchi 116.
Shuma amesema hakutakuwa na kiingilio katika tamasha hilo
ambalo linatarajiwa kuanza majira ya saa kumi na moja jioni na hivyo kuwaomba
wapenzi na mashabiki wa muziki kujitokeza kwa wingi katika tamasha hilo
linalodhaminiwa na Fastjet, Balozi za Ufaransa na Ujerumani, kinywaji cha Pepsi
na Total.
Kala Jeremiah analielezea onyesho hilo kama mazao ya kazi
nzuri aliyoifanya katika muziki wake “Nimepata faraja sana kualikwa kutumbuiza
kwenye world music day, inaonyesha ni kwa jinsi gani muziki wangu unakubalika
na kutambulika kitaifa na kimataifa”.
Shirika la ndege la Fastjet kupitia kwa Afisa Masoko Mtendaji
Lucy Mbogoro linajivunia kudhamini tamasha hilo likitumia nafasi hiyo kurejesha
shukran kwa Watanzania kwa mchango wao mkubwa katika shirika hilo kwa kuchagua
kutumia huduma zake za usafiri wa anga.
Mbogoro anasema “World Music Day ni fursa nzuri ya kukutana
na wadau wetu kwakuwa tamasha litawakutanisha watu wa mataifa mengi watapata
kujua huduma zetu katika wakati huu tunaoelekea kuanzisha safari za ndege za
kimataifa katika nchi za Afrika Kusini, Zambia na Rwanda”








