BATULI ATEMBELEA MAGONGO
MSANII wa filamu nchini Zaytun Kibwana 'Batuli' sasa atembelea magongo baada ya kupata matibabu ya mguu baada ya kuumia akiwa anatengeneza filamu 'Location'.
Msanii huyo ambaye anashindwa kutembea au kujisogeza ameweza kupata matibabu kwa kuwekewa kifaa maalumu, kitakachoweza kurudisha goti katika hali ya kawaida.
Akizungumza mara baada ya kuwekewa kifaa hicho chenye chuma, Batuli aliweka wazi kuwa ameanza kupata nafuu ingawa anatumia magongo kwa ajili ya kutembea na kusimama.
Alisema dokta ndiye aliyemshauri kutumia kifaa hicho kuliko kufanya upasuaji ambao ungempelekea kukaa kitandani kwa muda mrefu huku akishindwa kutembea.
"Sasa namshukuru mungu naendelea vizuri ingawa siwezi kutembea wala kusimama hivyo inanilazimu nitumie magongo, nimeweka kifaa hicho mguuni naamini nitapata nafuu muda si mrefu" alisema Batuli.
Alisema ghalama za hospitali ni kubwa hali iliyopelekea ashindwe kumudu pekee yake hali iliyosababisha aombe msaada kwa baadhi ya ndugu wanaomzunguka ili aweze kujitibu.
Batuli anasumbuliwa na mguu huo kwa muda mrefu, lakini umezidi baada ya kushtuka tena alipokuwa location hali iliyomsababisha kushindwa kutembea au kujisogeza.