KALA JEREMIAH -KUTOA SOMO LA KUPAMBANA NA RUSHWA
MSANII wa muziki wa Hip Hop nchini Kala Jeremiah aitaka jamii kupambana na kudhibiti mianya yote ya kupokea na kutoa rushwa inayoonekana kuwa ni adui wa haki na kurudisha maendeleo ya taifa nyuma.
Hayo aliyasema hivi karibuni jijini Dar es Salaam baada ya kutembelea Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU), alipopata nafasi ya kuzungumza na Mkurugenzi wa taasisi hiyo Dk. Edward Hoseah.
Alisema kuwa alipata nafasi ya kujadili masuala mbalimbali yanayotokana na rushwa na jinsi rushwa hiyo inavyotokea hususani katika sekta za maendeleo nchini.
Kutokana na majadiliano hayo alisema kuwa wamejadili pia mbinu mpya ya kukabiliana na tatizo hilo la rushwa ili kutokomeza tatizo hilo na kurudisha usawa katika jamii.
"Kila mtu katika jamii anawajibu wa kuzuia rushwa kama mwizi okoa jirani zako, zuia rushwa okoa jamii yako hii ndio hali pekee itakayoweza kukomesha rushwa nchini " alisema Kala.
Kala ambaye anatamba na kibao chake kinachojulikana kwa jina la Tambua Kujiuliza alisema kuwa kupitia nafasi yake aliyokuwa nayo katika sekta ya muziki anaamini kuwa mfano na kioo cha jamii kwa kuelimisha jamii yake kwa kutumia muziki ili kila mmoja aweze kupambana na rushwa.