MSANII wa muziki nchini Marekani, Rihanna amethibitisha kuwa ni miongoni mwa wasanii wadogo, waliopata mafanikio baada ya kumnunulia mama yake nyumba ya kifahari kwa dola za Marekani milioni 22, ambazo ni sawa na bilioni 35 za Kitanzania.
Rihanna amemnunulia mama yake jumba hilo la kifahari mjini Barbados, ambapo msanii huyo ndipo alipozaliwa na kukulia, ingawa hurudi nyumbani hapo kila mwisho wa mwaka kwa ajili ya kusherehekea sikukuu za Kristimas akiwa na familia yake.
Mbali na hilo, Rihanna ameandika historia nyingine baada ya kujaza mashabiki wengi katika shoo yake aliyoifanya katika uwanja wa mpira wa miguu nchini Afrika Kusini.
Msanii huyo ambaye yupo Afrika Kusini kwa ajili ya kufanya shoo yake ya 'Diamonds World Tour', ameweza kuvunja rekodi kwa kuujaza uwanja huo ambao hujaa katika mechi kubwa za soka hasa za kimataifa.
Kwa mujibu wa mtandao wa Entertainment Wise, tiketi zote za shoo hiyo zilimalizika na zaidi ya watu 67,000, walihudhuria shoo hiyo, hali iliyosababisha msanii huyo mwenye miaka 25 kuwa wa kwanza kuujaza uwanja huo na tiketi zote kumalizika.









