Google PlusRSS FeedEmail

MISS TANZANIA YAPIGWA STOP


Mashindano la Miss Tanzania 2014 yaliyokuwa lifanyike Jumamosi sasa halitafanyika hadi pale kesi ya msingi iliyozua mzozo baina ya wakurugenzi wa Kampuni ya Lino Agency inayoratibu mashindano hayo itakapomalizika.

Jana, mahakama ya hakimu mkazi Kisutu, Dar es Salaam ilitupa pingamizi la muda lililowasilishwa na mwanzilishi wa mashindano hayo, Hashim Lundenga akipinga maombi ya zuio la muda la kusimamisha mashindano yaliyotarajia kufanyika Jumamosi lilowasilishwa na mshirika wake, Prashant Patel.

Uamuzi huo ulitolewa jana na hakimu mkazi wa mahakama hiyo, Frank Moshi baada ya kusikiliza pingamizi hilo la awali lililowasilishwa na Lundenga kupitia wakili wake, Audax Kahendaguza.

Lundenga kupitia wakili wake aliwasilisha pingamizi hilo juzi akipinga maombi hayo yaliyowasilishwa na Patel ambaye ni mwanzilishi mwenza wa mashindano hayo pamoja na Lundenga.

Katika maombi ya Patel, aliiomba mahakama hiyo kutoa zuio la muda kwa mashindano hayo lililotarajia kufanyika katika Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.

Patel kupitia kwa wakili wake, Benjamin Mwakagamba aliiomba mahakama hiyo itoe zuio hilo ili kusubiri uamuzi wa kesi ya msingi aliyoifungua mahakamani hapo dhidi ya Lundenga. Katika pingamizi la awali, Lundenga alidai mahakama hiyo haina mamlaka ya kutoa amri hiyo inayoombwa, hati ya kiapo inayounga mkono maombi hayo ina upungufu, pia maombi yameletwa kabla ya muda.

Katika uamuzi wake, hakimu Moshi alikubaliana na hoja za wakili wa Patel, Mwakagamba kwamba mahakama yake ina mamlaka ya kusikiliza maombi ya zuio na kwamba yameletwa chini ya vifungu vinavyostahili.

Wakati wa usikilizwaji wa pingamizi hilo, wakili wa Lundenga alidai kwamba Patel amefungua kesi ya msingi kuhusu fedha na siyo mashindano hayo. Alidai katika hati ya makubaliano, walikubaliana kwamba siku tano kabla ya mashindano, mteja wake (Lundenga) angetakiwa kumpatia mshirika wake, Patel Sh12 milioni.

“Mheshimiwa, mdai kafungua kesi ya msingi Septemba 29, ikiwa ni siku 12 kabla ya mashindano na maombi ya zuio ameyaleta Oktoba 3, ikiwa ni siku nane kabla ya mashindano hayo. Hivyo, alitakiwa kusubiri kuona kama hatalipa au la,” alidai wakili huyo.

Mashindao ya Miss Tanzania yalirejeshwa rasmi 1994 baada ya kuzuiwa na Serikali na yamekuwa yakiratibiwa na Lino Agency ambayo yanamilikiwa kwa pamoja.

Mshindi wa mwaka jana, Happiness Watimanywa atalazimika kuendelea kusubiri kwa muda ili kumpata mrithi wake.

This entry was posted in

Leave a Reply

    Receive all updates via Facebook. Just Click the Like Button Below...

    Get This SpiceUpBlogging