Google PlusRSS FeedEmail

AMIGOLAS KUZIKWA LEO

Mwanamuziki wa bendi ya Ruvu Star inayomilikiwa na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Hamis Kayumbu Amigolas aliyefariki dunia usiku wa kuamkia jana baada ya kulazwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa siku tano, anatarajiwa kuzikwa leo saa 9:00 kwenye makaburi ya Kisutu, Dar es Salaam. Amigolas alikuwa anasumbuliwa na maradhi ya moyo kwa muda mrefu, lakini hali yake ilibadilika siku sita zilizopita na kulazwa kitengo cha moyo kabla ya kufikwa na mauti jana.

Kiongozi wa bendi ya Twanga Pepeta ambayo mwanamuziki huyo aliifanyia kazi kwa zaidi ya miaka 18 kabla ya kuhama, Asha Baraka alisema kuwa anachofahamu marehemu alikuwa na tatizo la moyo kwa miaka mitano iliyopita.

Akizungumza nyumbani kwa mama wa marehemu Kigogo Mburahati, Asha Baraka alisema, “Unajua wanzilishi wa bendi ya Twanga Pepeta wa mwanzo ni Luiza Mbutu, Jesca Charles, Robert Ega, marehemu Abuu Semhando na baadaye alikuja Amigolas mwaka 1997.

“Watu wasifikiri Amigo amekufa ghafla, amekuwa akisumbuliwa na moyo kwa muda mrefu, miaka mitano iliyopita, kwa wanaofahamu hawajashtuka kusikia hili kwa kuwa moyo wake ulishafikia kwenye hali mbaya, dozi yake ya dawa nilikuwa nanunua Sh450,000 kila mwezi,” alisema Asha Baraka.

Alisema, “Jumatatu alipelekwa Muhimbili na alilazwa kitengo cha Moyo, amedumu kwa siku tano kabla ya jana (juzi) saa tano na dakika 10 usiku kuaga dunia.”

Akimzungumzia Amigo, Baraka alisema, “Siwezi kusimama mbele za watu kuzungumzia mafanikio ya Twanga bila ya Amigo, nitakuwa ni mnafiki na mkosefu wa fadhila, Amigo ndiye aliyekuwa anatuunganishia matamasha yote ya nje ya nchi tuliyofanya, Omani tumeenda mara sita, yote ni yeye aliyefanikisha, tukaenda Marekani na nchi za Scandnavia.

“Matatizo yake ya moyo yalifanya tusimtumie sana kwenye muziki zaidi tulimpa umeneja wa bendi baada ya Abuu Semhando kufariki dunia.

“Aliondoka Twanga baada ya kuombwa na Mkuu wa Kikosi cha Ruvu JKT kilichoko Mlandizi, Pwani, Meja Charles Mbuge ili akaimarishe JKT Ruvu, aliwaomba watatu, Amigo, Victor Nkambi na Jojo Jumanne, ila Jojo alirudi Amigo na Victor walibaki, hadi mauti yanamkuta alikuwa yupo JKT,” alisema Asha Baraka.

Naye mama wa marehemu Amigo akizungumza na gazeti hili kwa uchungu huku akishindwa kujizuia kulia alisema, “Mwanangu ameondoka, ameondoka ameniacha sijui kama nitaweza kuishi, sidhani kama nina maisha marefu tena, nazika watoto wangu mimi nabaki, Amigo alinithamini, Amigo alinijali, Amigo hakuwahi kunidharau, Amigo umeondoka nani atanipeleka safari zangu, nani ataniita mama, Amigo nilikutegemea jamani mwanananguu!!!” alilia kwa uchungu.

Mpwa wa marehemu Rajabu Ahmed ambaye Amigo amefia mikononi mwake alisema, “Amigo hakuwa mkubwa katika familia, kulikuwa na wakubwa zaidi yake, lakini kutokana na tabia yake na ukarimu wake akajikuta familia inambebesha majukumu kwa kumtegemea kwa kila hali, ukimkosea anakwambia wazi, hakujua kuficha pale anapokwazika.”


Akizungumza kwa shida msibani maeneo ya Mburahati mke wa marehemu Joyce Amigolas, alisema kuwa madaktari walikuwa kwenye mpango wa kumfanyia upasuaji kitu ambacho hakikuweza kufanyika.


“Siwezi kuzungumza dada, niache unaona nilivyoachiwa mtoto mdogo, niseme nini mimi, ”alisema mkewe huyo aliyeachwa na mtoto wa miaka mitatu.

This entry was posted in

Leave a Reply

    Receive all updates via Facebook. Just Click the Like Button Below...

    Get This SpiceUpBlogging