Google PlusRSS FeedEmail

WAANDAAJI MISS TANZANIA WAJITATHIMINI

Mkurugenzi mtendaji wa Kampuni ya Lino International Agency Ltd, Hashim Lundenga juzi alikutana na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam na kuthibitisha kupokea barua ya Sitti Mtemvu ya kujivua taji la Miss Tanzania 2014.

Kampuni hiyo ndiyo waandaaji wa mashindano hayo ya Miss Tanzania. Sitti amelazimika kuvua taji hilo baada ya kuibuka mjadala mkali katika jamii kwa takriban mwezi mmoja kuhusu umri wake kwani anadai ana miaka 23 wakati nyaraka zake mbalimbali ambao wanadai zinaonyesha ana umri wa miaka 25 akiwa amezaliwa Mei 5, 1989.

Baada ya nyaraka hizo kusambaa katika mitandao ya kijamii, ikiwamo leseni yake ya udereva na hati yake ya kusafiria, msichana huyo aliibuka na kuonyesha cheti chake cha kuzaliwa kilichotolewa Septemba mwaka huu, kikionyesha kuwa amezaliwa Mei 5, 1991 na siyo 1989 kama baadhi ya nyaraka zake zilivyoonyesha.

Baadhi ya sifa za kushiriki shindano la Miss Tanzania ambazo mshiriki wa shindano hilo anatakiwa kuwa navyo ni pamoja na kuwa na umri usiozidi miaka 23 pia asiwe amezaa.


Kwa mujibu wa Lundenga, kutokana na uamuzi huo wa Sitti kujivua taji, nafasi yake sasa itachukuliwa na Miss Arusha, Lilian Kamazima ambaye alishika nafasi ya pili katika shindano la Redds Miss Tanzania lililofanyika Oktoba 11 mwaka huu kwenye ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.


Sisi tunaamini kwamba kitendo alichokifanya Sitti cha kujivua taji la Miss Tanzania ni funzo kwa waandaaji wa mashindano hayo kujitathmini upya na kuangalia mwenendo mzima wa mashindano hayo.


Tunasema hivyo kwa sababu inaonekana mshindi amekuwa akipatikana kwa kuangaliwa uzuri pekee bila kuzingatia sifa anazotakiwa awe nazo kwa mujibu wa sheria za mashindano ya dunia na pia kuangalia uwezo wa mshindi kuipeperusha bendera ya Tanzania kimataifa.


Ni wazi kitendo cha Sitti kujivua taji la Miss Tanzania ni dosari kubwa kwa mashindano kwani mshindi huwa ni mtu ambaye wasichana wadogo wangependa kujifunza kwake mambo mengi na hivyo kutumiwa kama kioo cha jamii.


Mshindi anapokuwa na kasoro yoyote, maana yake unawaambia wasichana wadogo wajifunze kasoro hizo na hali kadhalika unaiambia jamii kuwa kasoro hizo siyo mbaya.


Pia, hadi kufikia ngazi ya Miss Tanzania Sitti aliwanyima nafasi wasichana wengi wenye sifa kuanzia Kitongoji cha Chang’ombe hadi Miss Temeke kabla ya kuingia mashindano ya Miss Tanzania.


Waandaaji wa Miss Tanzania hawana budi kujitathmini, hasa katika kanuni zao za kupata washindi kuepuka fedheha kama hiyo ya safari hii ambayo haitoi taswira nzuri kwa shindano hilo kubwa nchini.


Tunahitaji mshindi wa Miss Tanzania ambaye ni raia mwema asiye na kasoro kama za kukiuka sheria za nchi kwa jinsi yoyote ile, lakini ambaye wasichana wadogo wa taifa hili watataka kujifunza kutoka kwake mambo mengi ya kimaisha, kielimu, kikazi na mengine ili shindano liwe na maana kwa jamii.

This entry was posted in

Leave a Reply

    Powered By Blogger

    Receive all updates via Facebook. Just Click the Like Button Below...

    Get This SpiceUpBlogging