Google PlusRSS FeedEmail

DIAMOND AWEKA REKODI, AWA CHACHU YA MAENDELEO KWA VIJANA

Mwanamuziki wa Tanzania, Diamond Platnumz amesema anajivunia kuandika historia mpya kwenye ramani ya muziki wa Afrika, baada ya kuvunja rekodi na kunyakua tuzo tatu za Channel O usiku wa kuamkia jana katika hafla iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Narsec Expo Centrem nchini Afrika Kusini.

Si hivyo tu, pia Diamond aliishangaza Afrika baada ya kunyakua tuzo kubwa ya Video Bora ya mwaka na kuwa msanii aliyeondoka na tuzo nyingi huku akiondoka na tuzo ya msanii bora Afrika Mashariki na mwanamuziki bora anayechipukia.

Diamond aliyeongozana na mama yake alisema, licha ya kuwashinda wasanii mahiri barani Afrika, anahisi bado hajafikia hatua anayostahili na kwamba anahangaika kuhakikisha anaifikia na kuendelea kukaa juu siku zote.

“Kuzoa tuzo tatu si jambo rahisi, ila nafahamu kuwa bado nina kazi kubwa kuhakikisha nafikia hatua ambayo naiota, najua kwamba nina kazi kubwa kuhakikisha nafika huko ila sitokata tamaa na bado natakiwa kuendelea kusimama katika nafasi niliyopo. Nina deni kubwa kwa Watanzania, nahitaji kupata tuzo nyingi zaidi zikiwamo za BET na nyinginezo,” alisema Diamond.

Nyota huyo aliyempiku mwanamuziki maarufu barani Afrika, Davido, alisema haikuwa rahisi kwake kushinda tuzo hizo ila anaamini mashabiki wake waliompigia kura na kujituma katika kazi ni kati ya vitu vilivyosababisha ushindi wake.

“Kiukweli, haikuwa rahisi kabisa, lakini kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu na kuungwa mkono na mashabiki, vyombo vya habari ndani na nje ya nchi iliwezesha Bongo Fleva yetu kuandika historia mpya kwenye ramani ya muziki wa Afrika,” alisema Diamond na kuongeza: “Hii inaonyesha ni jinsi gani umoja ni nguvu, pia inadhihirisha kuwa muziki wetu ukipewa sapoti na kipaumbele unaweza kufika mbali zaidi.” Afrika ilishuhudia Diamond akinyakua tuzo hizo na kumpiku Davido ambaye alikuwa akiwania vipengele vitano, huku mwanamuziki kutoka Afrika Kusini, Cassper Nyovest naye akinyakua tuzo tatu.

Wasanii wengine waliochukua tuzo hizo ni pamoja na DJ Clock, Tiwa Savage, K.O, Riky Rick, Burna Boy, Emmy Gee pamoja na Prince of Hip Hop A.K.A.

Mwanamuziki Kcee alisema Diamond ni kati ya wasanii wanaoibukia Afrika wenye vipaji na watakaoweza kuitangaza Afrika hapo baadaye.

“Napenda nikimwona anafanya shoo, ni kati ya wasanii wenye vipaji wanaoibuka hivi sasa na anavyoonekana ni kwamba hachoki na kile anachokifanya. Tulimwona alipotoa ‘Number One’, wengi walidhani alibebwa na Davido, lakini ameonyesha kwamba anaweza baada ya kutoa ‘Mdogo Mdogo’ na video yake mpya (akimaanisha ‘Ntampata Wapi’),” alisema Kcee.
Kcee aliyenyakua tuzo ya wimbo wa kushirikiana kupitia wimbo wake ‘Pull Over’, huku Tiwa Savage akifanikiwa kushinda tuzo kupitia wimbo wake wa ‘Eminado’.

This entry was posted in

Leave a Reply

    Receive all updates via Facebook. Just Click the Like Button Below...

    Get This SpiceUpBlogging