Google PlusRSS FeedEmail

ABDUL BONGE KUSAFIRISHWA LEO

Vilio na simanzi vimetawala katika tasnia ya muziki nchini baada ya kuondokewa na aliyekuwa mwasisi na meneja wa kundi la muziki la Tip Top Connection, Abdul Bonge, aliyefariki dunia ghafla Jumamosi jioni.

Bonge alifikwa na umauti alipokuwa akikimbizwa katika Hospitali ya Mwananyamala baada ya kusukumwa na kuanguka, alipokuwa akiamulia ugomvi wa vijana karibu na nyumbani kwao Magomeni Kagera.  Kwa mujibu wa msanii kutoka kundi la Tiptop Connection Ahmad Ally ‘Madee’, msiba upo Manzese Tip Top na taratibu za mazishi zinapangwa.

“Nimeumia sana kwa kweli, sikuwahi kufikiria na nilimwacha mzima wa afya wakati naelekea Zanzibar kikazi, hivi sasa ndiyo narudi, lakini tunatarajia kusafirisha kwenda Morogoro kwa ajili ya mazishi kesho (leo),” alisema Madee na kuongeza:

“Tangu niingie Tip Top Connection sikuwahi kutoka na nilikuwa nikimwambia Abdul Bonge kuwa siku yako haijulikani, leo imejulikana. Nisingekuwa mimi bila yeye, nilijivunia kuwa na yeye nilijiamini popote pale. Yeye nilimwona ni baba wa muziki wangu, sasa sijui nani atanielekeza nikikosea kuandika, atangulie kwa amani na mimi nitamfuata siku moja.”

Marehemu Bonge atakumbukwa kwa kazi yake nzuri ya kuwaibua wasanii kama Madee, MB Dogg, PNC, Pingu na Deso, K Sher, Z Anto, Tundaman na wengine wengi. Kabla ya kuachana na kazi hiyo, marehemu alipumzika kujishughulisha na muziki na kumpisha mdogo wake Babu Tale kuendelea na kazi hiyo.  Wasanii na watu mbalimbali mashuhuri nchini wameeleza kusikitishwa kwao na kifo cha muasisi huyo wa Kundi la Tip Top.

This entry was posted in

Leave a Reply

    Powered By Blogger

    Receive all updates via Facebook. Just Click the Like Button Below...

    Get This SpiceUpBlogging