VAN VICKER PROFILE
Ni ukweli usiopingika ukanda wa nchi za Afrika Magharibi ndiyo ukanda pekee barani Afrika ambao umepiga hatua kubwa katika filamu za maigizo.
Ukweli huo unadhihirika wazi ukiangalia kazi za wasanii wanaotoka ukanda huo hususani Ghana na Nigeria mafanikio waliyonayo ni makubwa mno ukilinganisha na wasanii wengine barani humu.
Miongoni mwa wasanii hao ni Van Vicker,ambaye kwa kiasi kikubwa amepiga hatua kubwa kimaendeleo kupitia tasnia hiyo.
Kabla ya kuyaanika mafanikio yake kwanza tuangalie alipotoka hadi kufikia hatua aliyopo kwa sasa.Historia inatuonesha kuwa kwanza jina lake kamili anaitwa Joseph Van Vicker na ni raia wa Ghana ambaye alizaliwa Agosti mosi 1977 na baba yake mzazi ni Mholanzi na mama yake ni raia wa Liberia.
Kwa bahati mbaya baba yake alifariki mapema sana wakati msanii huyo akiwa na umri wa miaka sita na kutokana na pigo hilo akalazimika kulelewa na mama yake tu na ndiyo maana hadi leo hii anamuhusudu mama yake akimuita shujaa wake.
Kwa upande wa shule tunaelezwa kuwa Vicker, alisomea katika shule ya Mfantsipim,ambako alisomea Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa Koffi Annan, akiwa na msanii mwenzake Majid Michel.
Baada ya kuhitimu masomo yake mwaka 2003 ndipo alipoamua kujitosa katika sekta ya burudani kama mtangazaji wa redio na Televisheni Metropolitan na mwaka huo huo akatokea kwenye kipindi kilichokuwa kikitengenezwa na kurushwa palepale Ghana kilichokuwa kikiitwa "Suncity" amabacho kilikuwa kikielezea maisha ya Chuo Kikuu
Katika kipindi hicho aliigiza kwa jina la LeRoy King Jr, akiigiza kama mwanafunzi wa chuo cha sanaa aliyezaliwa nchini Marekani na kwenda chuoni hapo Suncity kumalizia masomo yake.
Baada ya kufanya vizuri katika kipindi hicho ambacho kilikuwa na vipindi kumi Van Vicker akapata mwaliko kama msanii msaidizi katika filamu yake ya kwanza iliyoitwa "Divine Love" ambamo humo alikutana na wakongwe waliokuwa wakifanya vizuri wakati huo kama Jackie Aygemang na Majid Michael.
Tunaambiwa kuwa filamu hii ndiyo ilimfungulia njia msanii huyo na tangu kipindi hicho akaanza kupaa na kupata mafanikio makubwa aliyonayo.
Vicker anadaiwa kuwa ni mkali wa filamu za mahaba na kwamba ndizo zinampatia soko kubwa ndani ya soko la Nigeria ikilinganishwa na kwao Ghana.
Kwa upande wa familia tunaambiwa kuwa Vicker ni baba mwenye nyumba kwani ameoa na ana watoto wawili
Kimafanikio Vicker yupo juu kwani anamiliki kampuni inaitwa Sky & Orange ambayo inashughulika na matangazo ya biashara ana pia kampuni nyingine inayoitwa Babetown inayojihusisha na kuandaa matamasha mbalimbali pale Accra na ana bonge la salooni ya kiume aliyoipa jina la Babetown.
Katika huduma za kijamii msani huyo pia hayupo nyuma kwani ana mfuko unaoitwa Van Vicker Foundation ambao unajihusisha na kuinua vipaji vya vijana katika sanaa.
Mwaka 2008 akipewa tuzo muigizaji bora ya African Movie Academy Award, ikiwa ni baada ya mwaka huo huo kukabidhiwa tuzo msanii bora anayechipukia.
Pia wa tuzo mwaka 2009 aliweza kuibuka msanii bora Afrika kwa upande wa filamu na hivyo kukabidhiwa tuzo ya Afro-Hollywood Award