Google PlusRSS FeedEmail

SAJUKI KUZIKWA IJUMAA, MAKABURI YA KISUTU







Msanii wa filam nchini Juma Kilowoko 'Sajuki' amefariki Dunia jana katika hospitali ya Taifa Muhimbili alipokuwa amelazwa kwa ajili ya Matibabu , msanii huyo ambaye aliugua kwa kipindi kirefu alianza matibabu nchini na baadaye kupelekwa India.

Mei 13 mwaka jana Sajuki alienda nchini India kutibiwa baada ya kupatwa na maradhi ya tumbo na uvimbe katika ini na alianza matibabu katika Hospitali ya TMJ, Msasani, Dar es Salaam nakufanyiwa uchunguzi ambapo Hospitali hiyo ilithibitisha kwamba ili kufanikisha matibabu yake lazima apelekwe India lakini alishindwa kuifanikisha tiba hiyo kutokana na kushindwa gharama za matibabu kuwa kubwa.

Msanii huyo aliweza kupata fedha za matibabu kwa kuchangia na wadau pamoja na wasanii wa filamu nchini na kuweza kufanikisha safari yake ya kwenda nchini Indi kwa ajili ya matibabu

Sajuki aliweza kufika nchini India kwa ajili ya matibabu na baada ya muda aliweza kurejea nchini huku afya yake ikiendelea kuimarika siku hadi siku

Katika hali isiyo ya kawaida na ambayo haikutarajiwa siku za hivi karibuni msanii huyo alianguka jukwaani mjini Arusha wakati akijaribu kuwasalimia mashabiki, Sajuki alidondoka mjini Arusha alipokuwa anafanya tamasha kwa ajili ya kuwashukuru wananchi kwa kumchangia pamoja na kutafuta fedha nyingine ili aweze kurejea India kwa ajili ya matibabu yake mwezi uliopita.

Sajuki alirudishwa jijini Dar es Salaam na kufikishwa katika hospitali ya Amana ya jijini Dar es Salaam ambapo ripoti ya madaktari iliyothibitishwa na viongozi wa TAFF ilionesha kuwa msanii huyo amepata tatizo la kufeli kwa figo yake.

Kutokana na hali ya msanii huyo kuzidi kuwa mbaya ndugu pamoja na viongozi wa TAFF waliamua kumuhamishia msanii huyo katika hospitali ya Muhimbili kwa ajili ya uangalizi zaidi huku mipango ya kutafuta fedha za kumpeleka tena nchini India zikiwa zinaendelea.

Rais wa Shirikisho wa Filamu Tanzania Simon Mwakifamba (TAFF) alithibitisha kuwa safari ya maandalizi ya msanii huyo kwenda India ilikuwa imekamilika baada ya Serikali kukubali kugharamia gharama zote za kumsafirisha

Alisema mpango wa kumsafirisha huyo kwa ajili ya matibabu ulikuwa umeshakamilika kilichokuwa kikisubiliwa ni msanii huyo kupata nafuu na awe na uwezo wa kupumua bila ya kutumia mashine

Alisema kuwa asingeweza kusafirishwa na mipira ya kupumua na hiyo ndio ilikuwa ni sababu ya wao kusubili mpaka atakapopata nafuu

"Pamoja na jitihada zote tulizozifanya kuhakikisha tunaokoa maisha ya msanii mwenzetu zimeshindikana kwani mungu alimpenda zaidi na asubuhi ya leo  Sajuki ameiaga Dunia,"alimaliza kwa kusema Mwakifamba huku akionekana  ni mwenye huzuni kubwa.

Msiba huo umepokelewa kwa hali ya majonzi na masikitiko makubwa kwa baadhi ya wasanii wa filamu nchini, viongozi wa siasa pamoja na wadau mbalimbali , ambapo wamesema ni pigo kubwa kwenye tasnia hiyo


Naibu waziri wa wizara ya Mawasiliano January Makamba ni mmoja wa wanasiasa walijitokeza kwenye kufanya mchakato wa kumchangia Sajuki ili aweze kuikamilisha safari yake ya kwenda India kwa ajili ya matibabu.

" Kwa mara ya kwanza mimi niliingia studio kufanya nyimbo ya kuhamasisha na aliweza kupata matibabu na kuweza kupata nafuu, nilikaa naye na nikamsikiliza alikuwa anandoto nyingi za kupeleka sanaa katika ngazi ya kimataifa " alisema Makamba

Makamba alisema kuwa wakati Sajuki alipokuwa kwenye hali mbaya alijitahidi kwa kila hali kwa kuhakikisha kuwa anaweza kupona na kurudi tena katika hali yake ya kawaida lakini imeshindikana kwani Mwenyezi Mungu ameamua kumchukua.

Alisema kuwa mbali na juhudi za watu wengine walishuhudia juhudi zake  mwenyewe binafsi kwa kuiangaikia afya yake ingawa kila jambo mungu ndio anayepanga.


Naye Mbunge wa Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe "Hali ya Afya ya Sajuki ndiyo ilinisukuma sana kuanza kusaidia wasanii nchini kupata kipato stahili cha kazi zao." aliongezea kuwa  "Kifo chake kimeniondolea Mtu niliyemtazama kama kishawishi Cha Mimi kupigania haki za Watanzania walio kwenye (entertainment industry),"alisema Kabwe.

Mbali na hayo katibu mtendaji wa Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) Ghonohe Materego alisema kifo cha msanii huyo ni pigo kubwa kwenye tasnia ya filamu kwa kumpoteza msanii mahiri wa filamu

Alisema kuwa anatoa pole kwa familia ya Sajuki pamoja na wanafilamu kiujumla kwa kipindi kigumu walichonacho hivyo wanatakiwa wawe na moyo wa kushukuru kwa kila jambo.

Alitoa wito kwa wasanii wote ili kuwaenzi wapendwa wao ni lazima wayaenzi na kuyaendeleza mambo yote mazuri yaliyoachwa, kwa kufanya hivyo watakuwa wamewaenzi kwa vitendo.

Wakati huo huo msanii wa filamu Steven Nyerere alisema taarifa ya kifo cha msanii Sajuki amezipokea kwa mshtuko mkubwa kwani wamefunga mwaka kwa majonzi ya kuondokewa na wapendwa na kufungua tena mwaka kwa hali hiyo hiyo ya majonzi.

Alisema kuwa kila jambo linapangwa na mungu kwani sajuki aliumwa kwa muda mrefu na kauli yake ya mwisho ndio ambayo inamuumiza tangu alipopokea  taarifa za msiba wake.

"Steve  ndugu yangu nateseka sana bora nikapumzike", hii  ndio ilikuwa kauli yake ya mwisho kwangu inaniuma sana kwani tulijitahidi kupigania uhai wake ila mungu ndio kampenda zaidi" alisema Steve Nyerere

Steve aliongezea kuwa kwa hali hiyo yeye inamtisha sana kwani hajui itakuaje siku zijazo kutokana na mapigo yanayowakumba wanafamilia ya tasnia ya filamu mfululizo.


Naye msanii wa filamu Ray alitoa majonzi yake kwa kusema kuwa walijitahidi kuupigania uhai wake hata kwa kuwa naye bega kwa bega kwenye matamasha yaliyokuwa yameandaliwa kwa ajili ya kuchangia fedha za matibabu

Ray alisema kutokana na mapigo hayo wanayoyapata katika tasnia hiyo mungu anawakumbusha kwa njia hiyo wasanii kumrudia mungu, wamche mungu na kujiweka tayari muda wowote kwa jambo lolote lile.

Aliongezea kuwa wasanii wanatakiwa kumcha mungu na wasiwe watu wa starehe na kufanya hanasa, hivyo wanatakiwa kujua wanajukumu kubwa la kumcha mungu kila siku.

Naye Msanii wa Ushairi Tanzania Mrisho Mpoto maarufu kama Mjomba alisema kila mtu mwenye nyongo lazima atapokea taarifa hiyo kwa majonzi makubwa.

Alisema kuwa watanzania walionyesha juhudi kubwa ya kutaka kuokoa na kuupigania uhai wa Sajuki ila ndio imeshindikana hivyo ni pigo kubwa kwa wasanii na kwa watanzania kwa ujumla.

Mrisho aliongezea kuwa kuna kila sababu ya kutafakari matendo yao kwani kifo kinatumika kutukumbusha wajibu wetu na kuyaacha ya duni kwa kumrudia mungu

Marehemu  Sajuki alizaliwa mwaka 1986 mkoani Songea na ni mtoto wa nne katika familia yao na ana elimu ya kidato cha nne ambayo aliimaliza mwaka 2003 na alifika jijini Dar es Salaam mwaka 2005 na kuanza shughuli zake za kisanii ambazo aliendelea nazo mpaka mauti yanamfika.

Msanii huyo anatarajiwa kuzikwa kesho kutwa saa tano katika makaburi ya Kisutu, Dar es Salaam.Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi Amina!.


This entry was posted in

Leave a Reply

    Powered By Blogger

    Receive all updates via Facebook. Just Click the Like Button Below...

    Get This SpiceUpBlogging