Gwiji la tasnia ya filamu Swahiliwood Steven Kanumba ‘The Great’ amebainisha kuwa hakuna kitu rahisi popote pale, ili ufanikiwe ni lazima usote na kufikia unakotaka kwenda na hilo pia katika tasnia ya filamu lipo, akiongea katika uzinduzi wa chuo maalum kwa ajili ya mafunzo ya filamu Tanzania Film Training Center kilichopo Ubungo alisema kuwa elimu ni muhimu sana katika sanaa.“Nakumbuka mimi baada ya kujiunga na kundi la sanaa la Kaole Sanaa Group nilikaa zaidi ya mwaka mmoja bila kuonekana katika Televisheni, na nilikuwa natamani kweli hasa pale nilipokuwa nikiwaona akina Mashaka wakiigiza, lakini nafasi hiyo ilikuwa adimu kwangu lakini nilivumilia, na nyinyi mnahitaji uvumilivu ndio maana mpo chuoni hapa,”anasema Kanumba.Pia Kanumba alimpongeza Mkurugenzi wa Chuo hicho Emanuel Myamba ‘Pastor Myamba kwa kuwa na wazo nzuri la ufunguzi wa Chuo hicho akiamini kuwa kinaweza kuleta nidhamu kwa wasanii wanaoingia katika tasnia hiyo ya filamu, jambo lingine ambalo kwake ni furaha ni pale msanii aliyemkaribisha katika fani hiyo kufungua chuo hata kabla ya yeye kuwa na wazo hilo.
TFTC ni Chuo kilichofunguliwa kwa kuangalia maisha halisi ya mtanzania na kimezingatia gharama za masomo kuwa za chini na mtu yoyote anaweza kumudu kulipa gharama hizo kwa kozi, kozi moja kwa muda miezi mitatu ni fedha za kitanzania Tshs. 480,000/ tu mwanafunzi anasoma katika darasa la kisasa huku akipigwa na kiyoyozi, Hongera Myamba kwa kutambua umuhimu wa elimu katika filamu Swahiliwood.