Imebainika kuwa wana Hip Hop waliopo kwenye ‘piki’ kwa sasa, Emmanuel Simwinga ‘Izzo Business’ na Ibrahim Mussa ‘Roma’, wapo kwenye uhasama. Hawa wanaunga orodha ya wana Hip Hop wengine waliowahi kutokea Tanzania, Marekani na duniani kwa jumla, kuingia kwenye bifu la paka na chui. Habari kuwa Izzo na Roma hawaivi, zilianza kama uvumi wa mitaani kabla ya kila kitu kuanikwa kwenye jukwaa la Ukumbi wa Dar Live, Machi 11, 2012 Siku hiyo, kulikuwa na Tamasha la Mnanda dhidi ya Mduara, Izzo alishika kipaza sauti ili kuwasalimia mashabiki wake lakini katikati ya wimbo wake Riz One, alimuomba DJ asimamishe muziki na kutumia muda huo kumponda Roma
Katika maneno yake, Izzo alisema kuwa Roma ni mtoto mdogo kwake na kuongeza kwamba wakati wowote atamtoa nishai. Baada ya hapo aliendelea kuimba Riz One lakini aliposhuka jukwaani, mwandishi wetu alimuuliza Izzo sababu ya kumponda Roma. Katika majibu yake, Izzo alisema: “Nataka kumuonesha Roma kuwa mimi najua muziki kuliko yeye. Nimeshasikia mengi kwamba anatamba mimi kiwango kidogo kuliko yeye. Yule mtoto wa Kitanga hawezi kushindanisha muziki wangu na wake, nitamtoa nishai.” Alipoulizwa chanzo cha bifu lao, alijibu: “Yule mtoto aliwahi kuwa mshkaji wangu, baadaye akaanza kuchongachonga, eti mimi simuwezi. Kuanzia sasa simfagilii, ipo siku nitamtoa nishai. Nataka kila shabiki wangu na shabiki wa kweli wa Hip Hop ajue kwamba mimi na Roma hatuwezi kuwa washkaji, simfagilii.”
Roma ambaye katika majibu yake, alisema anajiamini kwenye muziki wake na hataki kusumbua akili yake kwa Izzo, kwani anaamini ni bwana mdogo kwake kimuziki. “Sitaki kuzungumza mengi lakini kwa kifupi ni kwamba anajisumbua. Mimi ni zaidi yake na hilo watu wote wanalijua. Kwanza huyo Izzo ni nani? Mimi simjui na sitaki hata kumjua,” alisema Roma.