EXTRA BONGO KUZINDUA UKUMBI
Bendi ya muziki wa dansi ya Extra Bongo ‘Wazee wa kizigo’ inatarajia kuzindua ukumbi wao wa Bongo Club uliopo Kimara Bucha, Dar es Salaam. Ukumbi huo ambao unamilikiwa na bendi hiyo utatambulishwa rasmi Julai Mosi mwaka huu ikiwa ni pamoja na gari lao kwa ajili ya kusafieisha wanamuziki wake katika maonyesho yao mbalimbali
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa bendi hiyo Ally Choki alisema wameamua kujenga ukumbi wao binafsi ili uweze kuwapunguzia gharama ambazo huzitumia kukodi ukumbi kwa ajili ya kutoa burudani
“Ukumbi huu utapunguza gharama ambazo tulikuwa tukizilipa kwa ajili ya kufanya burudani na tutakuwa tukifanya shoo kila ijumaa mara baada ya kuuzindua, huku siku nyingine ratiba zikibaki palepale” alisema
Pamoja na hayo alisema mara nyingi walikuwa wanatumia gharama kubwa kulipa katika kumbi wakati wao hawana vyanzo vingine vya mapato zaidi ya kutegemea viingilio ambayo haitoshi
Alisema anategemea ukumbi huo utakuwa na faida kwao kuweza kufidia hasara mbalimbali watakazokuwa wakizipata
Aliongezea kuwa siku hiyo ya uzinduzi pia watawatambulisha wanamuziki waliojiunga na bendi hiyo hivi karibuni ikiwa ni pamoja na rapa wao Frank Kabatano pamoja na staili mpya za uimbaji