MNYANGE atakayeiwakilisha Tanzania katika mashindano ya urembo ya dunia mwaka huu anatarajiwa kupatikana Jumamosi. Mwakilishi huyo atapatikana katika mashindano yaliyopewa jina la Redd's Miss World Tanzania yatakayofanyika katika Ukumbi wa 327 Club jijini.Akizungumza na Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Lino Agency ambao ndio waandaaji wa mashindano ya urembo nchini, Hashim Lundenga alisema mashindano hayo yanatarajia kushirikisha jumla ya warembo 10.Alisema warembo 10 ndio waliothibitisha kushiriki katika mashindano hayo ambaye mmoja wao ndio ataiwakilisha Tanzania katika mashindano ya Miss World yatakayofanyika Agosti, mwaka huu nchini China.Lundenga alisema kuwa wameamua kuchukua warembo waliowahi kushiriki katika mashindano ya Miss Tanzania katika miaka iliyopita, kutokana na mabadiliko ya ratiba ya mashindano kwani awali yalikuwa yanafanyika Desemba."Tumeamua kuchukua warembo ambao walishawahi kushiriki katika mashindano ya Miss Tanzania miaka iliyopita kwa kuwa mashindano yetu huwa yanaanza Mei na kumalizika Septemba," alisema.
Lundenga alisema mshindi katika mashindano hayo anatarajiwa kuzawadiwa sh. milioni 10 pamoja na kufanyiwa maandalizi yote ya kwa ajili ya matayarisho ya safari.Naye Meneja wa kinywaji cha Redd's, Victoria Kimaro, alisema wamejiandaa vizuri na mashindano hayo ambapo wanatarajia kuwa watapata mwakilishi mzuri.Alisema kuwa shindano hilo litakuwa kwa ajili ya watu maalum ambao wataalikwa na kutakuwa na burudani ya aina yake.