Google PlusRSS FeedEmail

BENDI ZAANZA KUTAMBIANA



Viongozi wa bendi zitakazopanda jukwaani katika Tamasha la Tanzania Live Music Festival (TMLF), wameanza kutambiana kwamba kila mmoja atafanya mambo makubwa siku hiyo.

Tamasha hilo linatarajia kufanyika kwa siku mbili, Ijumaa na Jumamosi katika viwanja vya Leaders ambapo bendi 12 zitaonesha umahiri wa kutoa burudani ya 'kufa mtu'.

Bendi zinazotarajia kupanda jukwaani siku hiyo ni FM Academia 'Wazee wa Ngwasuma', Akudo Impact 'Wazee wa Masauti', DDC Mlimani Park 'Sikinde Ngoma ya Ukae' na Msondo Music Band 'Baba ya Muziki'.

Nyingine ni Skylight 'Wazee wa Azonto', Mashujaa Music Band, Mashauzi Classic, Parapanda, Oryx, Wazee Sugu chini ya mkongwe King Kikii, Khadija Kopa na B-Band inayoongozwa na baba na mwana, Banana Zoro na Zahir Ally.

Akizungumzia tamasha hilo, Rais wa FM Academia, Nyoshi el Sadaat alisema ili kuhakikisha siku hiyo wanatoa burudani ya nguvu waliamua kwenda Zanzibar kwa ajili ya kujifua na kupata nguvu mpya.

"Tunategemea tutavurumisha burudani kwa kwenda mbele siku hiyo, hivyo tunawaomba wapenzi wa muziki wa dansi kujumuika nasi pale Leaders Klabu tucheze pamoja," alisema Nyoshi.

Naye kiongozi wa Akudo Impact, Christian Bela alisema wao ni vitendo tu siku hiyo kwani hana haja ya kuzungumza sana, isipokuwa amewataka mashabiki wake kujazana kwa wingi katika tamasha hilo kwani kuna vitu adimu amewaandalia.

Kwa mujibu wa mratibu wa tamasha hilo, Edwin Ngere kiingilio kitakuwa sh. 5,000.

Ngere alisema maandalizi ya tamasha hilo la aina yake, yamekamilika kwa asilimia 95 hivyo amewataka mashabiki wa dansi kutokea kwa wingi, kwani hiyo ni historia mpya inaandikwa nchini.

Tamasha hilo limedhaminiwa na Bussines Times, Redio Times na Global Publishers.

This entry was posted in

Leave a Reply

    Powered By Blogger

    Receive all updates via Facebook. Just Click the Like Button Below...

    Get This SpiceUpBlogging