DIVA wa filamu za kibongo Jacqueline Wolper anatarajia hivi karibuni kutoka na movi inayokwenda kwa jina la 'After Death'kwa ajili ya kumuenzi marehemu Steven Charles Kanumba
Akizungumza na jarida la Maisha jana jijini Dar es Salaam, Wolper alisema kuwa ameamua kutoka na filamu hiyo kwa sababu ya kumuenzi kwa vitendo msanii mwenzie marehemu Kanumba
Alisema filamu hiyo inaelezea maisha ya marehemu Kanumba baada ya kifo chake, ndani ya filamu hiyo ameigiza na watoto wawili ambao walikuwa wakiigiza na marehemu Kanumba
"Kwenye filamu hiyo nimeamua kuigiza na wasanii wengi ambao walishawahi kufanya kazi na marehemu kanumba, na nimeamua kufanya hivyo kwa sababu ya kumuenzi marehemu kwa vitendo na ukiangalia nimefanya naye kazi nyingi ikiwemo ile ya mwisho 'Ndoa yangu' hivyo nina kila sababu ya kufanya hivyo" alisema Wolper
Mbali na hayo alisema kuwa ameamua kujitolea kuwaendeleza Patrick na Jenifer ni watoto ambao walikuwa wakifanya kazi na marehemu Kanumba ili kuendeleza vipaji vyao kwani hakuna mtu aliyejitokeza kufanya hivyo
Alisema kuwa ni vizuri kuviendeleza vipaji vya watoto hao kwani mwenye marehemu alikuwa na ndoto ya kuinua vipaji chipukizi ili kuikuza tasnia ya filamu nchini Tanzania
"Kwa kuwaendeleza watoto hao kwangu mimi ni faraja kubwa kwani naamini sasa namuenzi kwa vitendo kwa sababu kitu ninachokifanya ndicho yeye alikuwa akipenda kukifanya kila wakati na alikuwa na ndoto ya kukuza vipaji vya chipukizi' alisema Wolper








