BAADA ya msanii wa filamu nchini Rose Ndauka kuripotiwa kufumaniwa akiingia gesti na msanii chipukizi wa muziki wa bongo fleva Nassoro Ayoub 'Dogo Nasry' huku akiwa amevaa baibui kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhani, mumewake mtaarajiwa Maliki Bandawe 'Chiwaman' amjia juu msanii huyo kwa madai ya kumchafua mpenzi wake.
Akizungumza jijini Dar es Salaam Chiwaman aliweka wazi kuwa msanii huyo Nasry ambaye alimuomba Rose aweze kushiriki kwenye video yake, walishindwa kufikia maamuzi kutokana na kiwango cha malipo kuwa madogo, na badala yake msanii huyo alimuomba wapige picha kama ukumbusho.
Alisema kuwa kitendo hicho cha kupiga picha na msanii huyo wakati wapo katika mazungumzo ya awali ya kukubaliana malipo ndizo picha alizotumia msanii huyo na kudai kuwa alikuwa naye nyumba ya wageni kitendo ambacho si cha kweli.
"Hawa wasanii wachanga wanatafuta umaarufu vibaya kwa kuwachafua watu, ilikuwa amemuomba Rose ashiriki kwenye video yake na ndipo walipokutana kwa ajili ya mazungumzo hayo na alikuwa na mdogo wangu sasa hapo masuala ya gesti yametokea wapi" alisema Maliki.
Aliongezea kuwa "kama nilikuwa sijui hicho kitu na kwa jinsi mambo yalivyokuwa ningeweza kumuacha mchumba wangu ninayempenda kwa dhati, ila msanii huyo alichokifanya siyo jambo sahihi, kwani alimuomba apige naye picha na Rose alikubali huku bila kujua nia yake ".
Maliki alisema kuwa huyo msanii anatafuta umaarufu kwa kuchafua majina ya watu wengine, kitu ambacho hakina mashiko kwenye jamii.