BARAZA la Sanaa la Taifa (BASATA) limefungia shindano la Miss Utalii Tanzania kwa muda usiojulikana. Akizungumza na waandishi wa habari Dar es salaam Jana Ofisa habari wa Baraza la sanaa la Taifa (BASATA), Agnes Kimwaga alisema mashindano ya hayo yamefungiwa kutokana na kushindwa kufanya tathimini ya mwaka 2012/2013 kwa muda uliokubalika baada ya kufanyika.
"Tumechukua jukumu hilo mpaka baraza litakaporidhishwa na mfumo wa uongozi wa Miss Utalii Organization utakapokuwa umeimarika na kujipanga upya kuendesha mashindano hayo," alisema Kimwaga.
Aliongeza kuwa licha ya baraza kuwakumbusha kufanya tathimini ya maandishi kwa barua yenye kumbukumbu namba BST/MTT/BJ/09 ya Agosti 5, mwaka huu yenye kichwa cha habari tathimini ya Miss Utalii 2012/2013 waliendelea kushindwa kutimiza agizo hilo.
Alisema sababu nyingine zilizofanya BASATA kuyafungia mashindano hayo ya Miss Utalii Tanzania 2012/2013 kukiuka masharti, kanuni na miongozo ya taratibu za uendeshaji mashindano ya urembo kama zilivyoweka na serikali kupitia BASATA.








