RAIS wa Shirikisho la Wasanii wa Filamu Tanzania (TAFF), Simon Mwakifamba amekanusha baadhi ya uvumi unaovumishwa na baadhi ya wadau wa filamu juu ya kujipatia kipato kitakachotokana na kuzindua taasisi ya Marehemu Steven Kanumba iliyopewa jina la 'Kanumba The Great Foundation'.
Ambapo hivi karibuni kumeibuka uvumi unaodai kuwa kamati inayosimamia uzinduzi wa filamu hiyo imejiwekea mazingira ya kujiingizia kipato, kwa kuandaa tamasha hilo litakalofanyika Dar Live jijini Dar es Salaam, huku kiingilio kikiwekwa wazi.
Akizungumza na Pro-24 njia ya simu, Mwakifamba amekanusha habari hizo na kudai kuwa hazina ukweli wowote kwani lengo la kuzindua Foundation hiyo ni kutafuta kipato kwa ajili ya kuendeleza taasisi hiyo yenye lengo la kusaidia vipaji chipukizi.
"Kila foundation inayoanzishwa lazima iwekewe mikakati ya kuiendeleza na hakuna taasisi inayoendelea bila ya kuwa na kipato, hivyo kuandaa tamasha hilo ni moja ya kutafuta kipato ili kuisaidia foundation hiyo kujiendesha" alisema Mwakifamba.
Kutokana na hilo familia pamoja na kamati ambayo ndiyo inayosimamamia maandalizi yote ya siku ya leo imeweka mikakati ya kuendeleza jambo hilo ikiwa msingi wake ni kumuenzi Kanumba kwa Vitendo.
Ambapo Mwakifamba amesisitiza kuwa Kanumba alikuwa ni msanii pekee aliyekuwa mstari wa mbele kuibua vipaji chipukizi hivyo kwa kupitia Foundation hiyo itaibua vipaji chipukizi huku akiweka wazi kuwa watafanya kazi nyingi za filamu kama marehemu angeweza kuzifanya.
Pamoja na hayo aliweka wazi kuwa kuhusu viingilio vitakavyotolewa vyote vitakuwa chini ya usimamizi wa kamati, ingawa foundation hiyo inasimamiwa na familia ambapo alieleza kuwa wao kama wadau wa filamu wameweza kutoa ushauri kwa familia hiyo kutafuta watu wenye ujuzi na uwezo wa kuendesha foundation hiyo ili iweze kuendelea na kufika mbali.
"Tumetoa ushauri kwa familia kuwa watafute watu wenye uwezo wa kuendeshe foundation hiyo ili kuiendeleza vinginevyo haitoweza kufika mbali, lakini familia imezingatia hilo" alisema Mwakifamba.
Taasisi hiyo inatarajia kuzinduliwa leo tarehe 7 April ikiwa sambamba na maadhimishi ya miaka miwili tokea kufariki kwa Kanumba.








