Google PlusRSS FeedEmail

RUGE AJIWEKA WAZI



Mkurugenzi wa Kituo cha Vipaji Tanzania (THT), Ruge Mutahaba amesema taasisi hiyo ni sehemu ya mikakati ya kukuza vipaji vya wasanii, na kamwe wanafunzi wake hawahusiani na mambo binafsi yanayowahusu viongozi.


Ruge aliyasema hayo wakati wa hafla fupi ya kumuaga msanii Amini Mwinyimkuu aliyekuzwa na kituo hicho kwa muda wa miaka tisa iliyofanyika makao makuu ya THT juzi jioni.


Alisema chuo hicho kinachochukua vijana zaidi 100 kila mwaka, kinatoa mchango mkubwa kwa jamii na hivyo huharibu taswira yake wakati mambo binafsi yanapoingizwa na kuwahusisha moja kwa moja wasanii wanaotokea THT.


“Inapofika mahali kuna vurugu, vita ambazo zinamhusu mkurugenzi, kwa bahati mbaya wasanii kutoka katika lebo hii huingizwa katika mikasa ya ajabu na hilo huwaumiza sana. Mara nyingi wanateseka bila ya kuhusika kwa namna yoyote ile na hiyo imetokea siyo mara moja ama mbili. Acheni hiki kitu hakiwahusu hawa. Wanifuateni mimi mwenyewe,” alisema Ruge.


Ruge, ambaye pia ni mkurugenzi wa vipindi na uzalishaji Clouds Media Group, alisema amekuwa akipambana na hali hiyo, lakini inapofikia hatua fulani, wasanii wakajituma na kuweza kupata lebo nyingine, inakuwa ahueni kwa THT kuendelea kuzalisha vijana zaidi.


“Ninafurahi hasa ninapoona msanii akaweza kusimama na akashinda majaribu yote haya na mpaka akapata lebo mpya na kuanza kupiga hatua ya kujitegemea lazima nimshukuru Mungu, na wote ambao walisaidia. Nia yetu ni kuwapa daraja na nilishawaambia kwamba itafikia hatua nitawaachia wakajitegemee,” alisema.


Alisema lebo hiyo inafahamika kwamba ni familia, hivyo ikihusishwa na mtu mmoja inaathiri wengi, kwani wapo wanaotumia lebo hiyo kutengeneza kazi mbalimbali kwa ajili ya kuendeleza muziki Tanzania.


“Akina Davido, Diamond wanarekodi hapa. Hakuna anayelipa hii ni sehemu ya mafunzo, wengine wanajua kwamba hii ni sehemu ya wanafunzi, lakini hii ni kwa ajili ya wasanii wote, ni nyumba ya vipaji. Ninachotaka kuona ni watu wanabadilisha mtazamo wao kuhusu THT ibaki kuwa kama shule,” alisema Ruge.


“Amini endelea kupenda kile unachopenda kufanya. Linah naye amekwenda kwenye lebo nyingine ya No Fake Zone, Amini na wewe unakwenda DME Company Limited. Barnaba naye yupo mbioni. Siyo kwamba tunafukuza waliopo, ila tunataka kuendelea kuzalisha vipaji vipya,” alisema.


THT imemuaga rasmi Amini ambaye ni miongoni mwa wasanii wanaotokea THT baada ya kuishi kwa zaidi ya miaka tisa.

This entry was posted in

Leave a Reply

    Powered By Blogger

    Receive all updates via Facebook. Just Click the Like Button Below...

    Get This SpiceUpBlogging