Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kama msimamizi na mratibu wa sekta ya Sanaa nchini linapenda kutoa pongezi za dhati kwa Msanii wa muziki wa kizazi kipya Nassib Abdul maarufu kama Diamond kwa kushinda tuzo tatu kwa mkupuo za CHOAMVA zinazoendeshwa na kituo maarufu cha luninga cha Channel 0 chenye makao makuu yake Afrika Kusini.
Tuzo alizoshinda Diamond ni pamoja na Most Gifted East African Artist, Most Gifted Afro Pop video na ile ya Most Gifted New Comer.
Kushinda kwa Diamond katika tuzo hizo kubwa barani Afrika na kuwashinda wasanii wengine wenye ‘majina makubwa’ ni ishara kwamba muziki wetu unakubalika ndani na Baraza linatoa wito kwa wasanii na wadau wote wa muziki kuzidisha ubunifu, bidii na weledi katika kazi wanazozifanya ili wasanii wengi zaidi waweze kuchomoza katika tuzo na majukwaa mbalimbali ya kimataifa kwa lengo la kujitangaza na kukuza soko la kazi zao kimataifa.
Aidha, Baraza linaendelea kuwakumbusha na kuwasisitiza wadau wa muziki na Sanaa kwa ujumla hususan wakuzaji Sanaa (mapromota) kuendelea kujenga mazingira rafiki kwa wasanii wetu kufanya kazi kwa ubora na weledi lakini pia kwa upendo na furaha ili kujenga daraja zuri kwa wasanii wengi zaidi kung’ara kwenye ngazi za kimataifa.
Ni imani ya Baraza kwamba, ushindi huu wa kihistoria wa Diamond utakuwa chachu kwa wadau wote wa Sanaa nchini hususan wasanii katika kujituma na kuhakikisha hawaridhiki na mafanikio waliyonayo.
Ni matumaini ya Baraza kwamba wasanii na wadau wote wa Sanaa wataendelea kutambua umuhimu wa kufuata sheria, kanuni na taratibu za uendeshaji sekta sambamba na kutambuliwa na Serikali.
Sanaa ni kazi, tuipende na kuithamini
Godfrey Mngereza
KAIMU KATIBU MTENDAJI