Mwigizaji Dotnata wiki iliyopita alifanyiwa upasuaji mkubwa kutokana na matatizo ya tumbo yaliyokuwa yakimsumbua ghafla na kulazwa katika Hospitali ya THI iliyopo Kinondoni, jijini Dar es Salaam."Namshukru kwanza Mungu wangu, pili ni hawa madaktari waliofanikisha zoezi hili na kunirudisha katika hali yangu ya kawaida, sasa naendelea vema. "Kwa taarifa aliyonipatia daktari, ninaweza kuruhusiwa na kurudi nyumbani kwa ajili ya mapumziko muda wowote huku nikiendelea na matumizi ya dawa, lakini kwa sasa nipo safi kabisa na hawa madaktari ni mabingwa na wametoka nje kwa ajili ya kazi hiyo tu," alisema Dotnata.
Kutokana na upasuaji huo, Dotnata amesema anatakiwa kupumzika kwa muda wa miezi sita bila kufanya kazi yoyote nzito wala haruhusiwi kuendesha gari. Kwa mantiki hiyo, hata kuigiza atahitaji kuigiza sehemu zisizo na purukushani zinazoweza kufanya apate matatizo. Mwanaspoti linampa pole kwa maradhi yanayomsumbua.