
Jeshi la Polisi mkoani Tanga, limefanikiwa kukamata nakala 400 feki za filamu ya Ngema, mali ya msanii Manaiki Sanga iliyoingia mtaani wiki iliyopita.
Habari za uhakika zilizotua mezani kwa Maskani Bongo zilisema kuwa shehena ya CD hizo zilikamatwa na askari wa kituo cha Mombo na baadaye mtuhumiwa huyo ambaye hakufahamika jina lake, alipelekwa kituo kikuu cha Polisi Korogwe kwa ajili ya kufanyiwa utaratibu wa kurejeshwa Dar kukabiliana na tuhuma dhidi yake.
mujibu wa Manaiki, mtu huyo ni mfanyabishara na alikuwa amekuja Dar kununua filamu hiyo kopi mia moja, lakini baada ya kufanya hivyo alizichakachua na kuzalisha zingine mia nne, ambazo Polisi walizishtukia kwa vile hazikuwa na stika ya TRA.
Baada ya kukamatwaa na kubanwa kwa nini DVD hizo hazina alama ya TRA, alikiri kuwa ni kweli alichakachuaa alipokuwa Dar kwenye mitambo maalum ya kudurufu kazi za wasanii ndipo Polisi hao walipompigia Manaiki simu kumfahamisha juu ya tukio hilo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga Costantine Masawe, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema aliagiza kijana huyo kupelekwa kituo kikuu cha Polisi Korogwe kwa ajili ya kufanyika taratibu za kupelekwa Dar tayari kwa kuandaliwa mashtaka ya kuiibia Serikali pamoja na wasanii.
Aidha Kamanda huyo alitoawito kwa watu wanaoiba kazi za wasanii kuacha tabia hiyo mara moja kwa vile zinazorotesha uchumi wa nchi kupunguza kipato cha msanii husika.







